Creation Science Information & Links!
Zaburi 1, 51, 100 & 150
Psalms 1 • 51 • 100 • 150 - in Swahili (Kiswahili)
Zaburi 1

Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.   Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.   Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.   Sivyo walivyo wasio haki; Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.   Kwa hiyo wasio haki hawatasimama hukumuni, Wala wakosaji katika kusanyiko la wenye haki.   Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki, Bali njia ya wasio haki itapotea.
 

Zaburi 51

Ee Mungu, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu.   Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu.   Maana nimejua mimi makosa yangu Na dhambi yangu i mbele yangu daima.   Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, Na kufanya maovu mbele za macho yako. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo, Na kuwa safi utoapo hukumu.   Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani.   Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni; Nawe utanijulisha hekima kwa siri,   Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji   Unifanye kusikia furaha na shangwe, Mifupa uliyoiponda ifurahi.   Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu; Uzifute hatia zangu zote.   Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu   Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.   Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi.   Nitawafundisha wakosaji njia zako, Na wenye dhambi watarejea kwako.   Ee MUNGU, Mungu wa wokovu wangu, Uniponye na damu za watu, Na ulimi wangu utaiimba haki yako.   Ee Bwana, uifumbue midomo yangu, Na kinywa changu kitazinena sifa zako.   Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa, Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.   Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.   Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako, Uzijenge kuta za Yerusalemu.   Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki, Na sadaka za kuteketezwa, na kafara. Ndipo watakapotoa ng'ombe Juu ya madhabahu yako. -
 

Zaburi 100

Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote;   Mtumikieni Bwana kwa furaha; Njoni mbele zake kwa kuimba;   Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu; Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake; Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.   Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru; Nyuani mwake kwa kusifu; Mshukuruni, lihimidini jina lake;   Kwa kuwa Bwana ndiye mwema; Rehema zake ni za milele; Na uaminifu wake vizazi na vizazi.
 

Zaburi 150

Haleluya. Msifuni Mungu katika patakatifu pake; Msifuni katika anga la uweza wake.   Msifuni kwa matendo yake makuu; Msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake.   Msifuni kwa mvumo wa baragumu; Msifuni kwa kinanda na kinubi;   Msifuni kwa matari na kucheza; Msifuni kwa zeze na filimbi;   Msifuni kwa matoazi yaliayo; Msifuni kwa matoazi yavumayo sana.   Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana. Haleluya.


Psalms 1 • 51 • 100 • 150
http://www.creationism.org/kiswahili/saPs1_51_100_sw.htm

Hoja kuu:  Kiswahili
www.creationism.org